Mwanamuziki wa Bongo Flava, Aslay amesaini rasmi na lebo Sony Music Entertainment Africa yenye makazi yake Afrika Kusini ambapo kazi ya lebo hiyo ni kusambaza kazi za wasanii.

Aslay anaungana na wasanii wengine wa Bongo Flava waliopo chini ya lebo hiyo ambao ni Ommy Dimpoz, Abigail Chams na Young Lunya.

Msanii huyo ambaye amesaini mkataba huo akiwa Johannesburg nchini Afrika Kusini, alisema ni furaha kwake kutangaza ushirikiano huo ambao si tu utamnufaisha yeye bali ni Bongo Flava kwa ujumla.

“Kwani mtandao wa kimataifa wa Sony Music Africa utaruhusu sauti yangu na muziki ninaowakilisha kutangazwa kimataifa na ninajivunia sana hatua hii katika taaluma yangu.” alisema Aslay.

Kwa Upande wake Mkuu wa Sony Music Afrika Mashariki, Christine “Seven” Mosha, alisema anajivunia kuwa na msanii hadhi ya Aslay kuungana nao.

“Ni mwimbaji na mtunzi wa kipekee ambaye ametetea aina ya Bongo Flava kote barani Afrika na sasa duniani kote, tunafurahi kushirikiana naye ili kuleta kipawa chake cha ajabu na muziki masikioni mwa mashabiki wengi kadiri tuwezavyo ulimwenguni.” amesema Seven.

Aslay ana utajiri wa mashabiki kwenye mitandao ya kijamii akimiliki wafuasi milioni tano (Instagram), milioni mbili (Facebook) na milioni moja kwenye chaneli yake ya YouTube.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *