Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia askari wawili wa Kikosi cha Anga pamoja na mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Moku kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa mafuta ya ndege.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema tukio hilo lilitokea Machi 17, mwaka huu kwenye hanga la Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius (JNIA).

Kamanda Sirro amesema Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usalama uwanjani hapo, walimkamata Iddy Nyangasa (42) mkazi wa Vingunguti kwa Mnyamani ambaye ni mlinzi wa Moku baada ya kuiba lita 38 za mafuta ya ndege kutoka kwenye ndege yenye namba za usajili 5H-MWF aina ya DASH 8-Q 300 mali ya ATCL iliyokuwa kwenye hanga hilo kwa ajili ya matengenezo.

Ameongeza kuwa baada ya ukaguzi wa kina na wahandisi wa ATCL, ilibainika jumla ya lita 220 ndizo zilizoibwa kutoka ndege hiyo.

Sirro amesema baada ya tukio hilo, uchunguzi wa kina ulifanyika na kubaini mtandao huo wa wizi wa mafuta ya ndege pia unahusisha askari polisi wa Kikosi cha Anga ambao ni Koplo Bahati Msilimini na Konstebo Benaus Mkama.

Pia amesema askari hao wamekamatwa kwa uchunguzi zaidi na mara tu uchunguzi utakapokamilika, watuhumiwa wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *