Askari wawili wanaotuhumiwa kuiba mafuta ya ndege ya Kampuni ya ATCL, kwa kushirikiana na walinzi wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao na wenzao wawili walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.

Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Koplo Bahati Msilimini (33), PC Benaus (34), Iddi Nyangasa (42) na fundi wa ndege, Ramadhani Mwishehe (52).

Katuga alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka  mawili, shtaka la kwanza kula njama na shtaka la pili hujuma dhidi ya Serikali.

Alidai katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi mosi na Machi 17 mwaka huu maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere walikula njama ya kutenda kosa la uhujumu uchumi.

Katika shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa kati ya tarehe hizo, wakiwa na nia ya kuhujumu manufaa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, bila uhalali walitoboa na kuchota mafuta ya ndege lita 280.6 kutoka kwenye ndege JET A1 ya ATCL yenye namba za usajili 5H\MWF-8Q-300.

Katuga alidai kitendo hicho kilizuia utoaji wa huduma muhimu ya usafiri wa ndege.

Hata hivyo wakili huyo alidai upelelezi haujakamilika na hakuna kibali chochote kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Source: Mtanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *