Mwanamuziki nyota wa Bongo fleva, Alikiba anatarajia kuanzisha lebo ya muziki itakayoitwa kwa jina la ‘Kings Music’ itakayohusika na kumiliki na kuwasimamia wasanii watakaokuwa chini ya lebo hiyo.
Hayo yamesemwa na mwanamuziki mkongwe wa Bongo fleva, Abby Skillz hivi karibuni wakati akielezea sababu ya kumfanya kuhama kwao Kariakoo na kuhamia nyumbani kwa Alikiba maeneo ya Tabata.
Abby Skillz amesema kuwa mpaka sasa labo hiyo imeshasaini wasanii kumi ila yeye ni msanii wa kwanza kabisaΒ kusaini chini ya uongozi wa Alikiba na kusema angeweza kuwataja wasanii wengine ambao tayari yameshadondosha wino lakini itakuwa si vyema hivyo muda utakapofika Alikiba mwenyewe ataweka wazi hilo.
Abby Skillz ambaye sasa anatamba na wimbo wake ‘Averina’ aliowashirikisha Alikiba na Mr Brue amesema hivi karibuni lebo hiyo itaanza kazi kwani mwaka huu itaanza kazi rasmi chini ya uongozi wa Alikiba.
Alikiba akifungua lebo hiyo ataungana na wasanii wengine ambao wana lebo zao za muziki mmoja wapo akiwa mpinzani wake kwenye sekta ya muziki Bongo, Diamond Platnumz anayemiliki lebo ya WCB pamoja na Ommy Dimpoz anayemiliki lebo ya PKP.