Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ametaka viongozi wa chama hicho kuitisha kikao cha Kamati Kuu ili kujadili namna ya kudhibiti vitendo vya kuwakamata viongozi wa chama hicho vinavyofanywa na wakuu wa mikoa na wilaya.

Lowassa amesema hayo juzi wakati wa futari aliyoindaa kwa madiwani na viongozi wa Chadema na wakazi wa Dar es Salaam iliyofanyika Mikocheni.

Amesema hayo wakati viongozi wa Chadema, akiwamo Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye walizuiwa kutembelea miradi ya maendeleo kwa madai kuwa kabla ya ziara hiyo, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alifanya kikao cha chama katika jengo la Serikali.

Meya huyo alikamatwa kwa amri ya mkuu wa Wilaya ya Ubungo na kukaa mahabusu kwa saa 48.

Mbali na Jacob, Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Likindikoki, diwani wa viti maalumu Kata ya Ngarenaro, Happiness Charles na diwani wa viti maalumu Kata ya Olorieni, Sabrina Francis walikamatwa na polisi kwa sababu ambazo hadi sasa hazijawekwa wazi.

Calist Lazaro ambaye ni meya wa Jiji la Arusha naye alijikuta akisekwa rumande kwa amri ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali wakati akijiandaa kupeleka rambirambi Shule ya Lucky Vincent iliyopoteza wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa gari katika ajali iliyotokea wilayani Karatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *