Familia ya rapa mkubwa nchini Afrika Kusini aliyeuawa kwa kupigwa risasi, Kiernan Forbes almaarufu AKA imetoa taratibu za mazishi za staa huyo ambaye atazikwa Februari 18, 2023.

Taarifa hizo zimeeleza kwamba kwa kuwa AKA alikuwa kipenzi cha wengi, shughuli maalum ya kuuaga mwili wake, zitafanyika katika Ukumbi wa Sandton Convention Centre Ijumaa ya Februari 17, 2023 ambapo tiketi kwa watakaotaka kuhudhuria, zitaanza kupatikana mitandaoni.

Familia hiyo imeongeza kuwa kwa wale ambao watashindwa kufika kwenye ukumbi huo, watapata nafasi ya kutazama shughuli nzima ‘live’ kupitia akaunti ya Youtube ya marehemu AKA ya Akaworldwide.

Taarifa zimeongeza kuwa kwa sasa, familia imemteua baba wa marehemu, Tony Forbes kuwa msemaji wa familia katika kipindi chote cha msiba.

Mbali na hayo, taarifa hiyo pia imeeleza kwamba Bongani Mahosana almaarufu kama Murdah Bongz, mume wa Dj Zinhle, mwanamke aliyezaa na marehemu AKA mtoto mmoja wa kike aitwaye Kairo, hataruhusiwa kushiriki kwenye msiba huo kwa namna yoyote kutokana na taratibu za kimila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *