Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amezindua kiwanda cha mabati cha ALAF kanda ya kati mjini Dodoma.

Kampuni ya ALAF (Tanzania) imefungua tawi lake jipya Mkoani Dodoma ikiwa ni kutekeleza maagizo ya Sera ya Viwanda kwa vitendo na kusogeza huduma kwa wananchi baada ya kufanya hivyo katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha. Tawi hili limezinduliwa tarehe Septemba 9, 2017 Kizota, Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema “Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali yetu inafanya kila linalowezekana kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwekeza kwa kulinda mitaji yao kupitia kuondoa ushindani usiokuwa wa haki hasa unaotokana na baadhi ya wafanya biashara kudanganya thamani ya bidhaa za bati zinazoingizwa toka nje ya nchi na kulipa kodi pungufu, kudhibiti uingizaji wa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zaidi kulinda amani na maelewano yaliyopo baina ya Serikali na wadau mbalimbali ili kujenga ustawi wa nchi yetu.

Waziri Mwijage aliendelea kwa kusema “Napenda kuwashukuru Kampuni ya ALAF (Tanzania) Ltd kwa kutekeleza vizuri maelekezo ya Sera ya Viwanda kwa vitendo na kusogeza huduma zao kwa wananchi wa Dodoma baada ya kufanya hivyo katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha.”

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya ALAF, Dipti Mohanty alisema “uwekezaji huu wa Dodoma ni wa thamani ya shilingi bilioni tatu ukiajiri watu 15 moja kwa moja na wengine zaidi ya 100 ajira zisizo za moja kwa moja kama kupakia na kushusha bati, kusafilisha bati, huduma za maji, stationary n.k.”

 Pia aliongeza kwa kusema “ALAF inakumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo uagizaji wa bidhaa sizizokidhi viwango unaofanywa na makampuni mbalimbali na pia ukwepaji wa kodi, kupelekea serikali kukosa mapato stahiki na walaji kutumia bidhaa zilizo chini ya viwango na hii hupelekea kukatisha tama wawekezaji wa ndani ambao wanajitaidi kuzalisha bidhaa zenye ubora na kulipa kodi zote stahiki.

Meneja wa ALAF kanda ya kati, Grayson Francis Mwakasege akizungumza jambo katika hadhira iliyofika kwa ajiri ya uzinduzi wa kiwanda cha mabati cha ALAF tawi la Dodoma kwa ajiri ya kuhudumia mikoa ya kanda ya kati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *