Zuma ateua tume ya kuchunguza ufisadi Afrika Kusini

0
29

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ameteua Tume ya Uchunguzi wa madai ya muda mrefu kuhusu ufisadi nchini humo.

Taarifa ya Zuma kwa vyombo vya habari ilisema Jaji Mkuu, Mogoeng Mogoeng ndiye aliteua jina la Naibu Jaji Mkuu Raymond Zondo na akampa rais ambaye alimtangaza kuongoza tume hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama Kuu ya Gauteng Kaskazini kumtaka Zuma afanye hivyo katika muda wa siku 30 kuanzia Desemba 14, 2017.

Tangazo hilo limekuja wiki mbili baada ya Zuma kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Juu uliomuamuru kuteua tume. “Nimekata rufaa dhidi ya amri ambazo kwa kiasi kikubwa zimejenga mwendelezo fulani kwa Ofisi ya Rais wa Jamhuri na kwa dhati yanahitaji uhakika wa kisheria,” alisema.

Rais amesema tume itakuwa na jukumu la kufichua siyo tu mwenendo wa baadhi, lakini wote wanaoweza kuwa wamehusika kulisababisha taifa au sehemu yake liathirike kwa kudhibitiwa na nguvu zilizo nje ya serikali.

Mkaguzi Mkuu wa Mali ya Umma wa zamani Thuli Madonsela alimuelekeza Rais Zuma aunde tume ya uchunguzi katika Ripoti ya Taifa Kuwekwa Mfukoni iliyoandaliwa baada ya kuchunguza madai lukuki dhidi ya familia ya Gupta, mtoto wa rais Duduzane Zuma na watu wengi walioko karibu na mkuu wan chi.

Kisha mwanamama yule aliagiza Jaji Mkuu Mogoeng Mogoeng ateue jaji kuongoza tume kwa kuwa Rais Zuma alituhumiwa kuhusika katika mtandao huo.

Juzi Madonsela alisema ingawa anapokea uamuzi huo kwa mikono miwili, anasikitishwa kutokana na ukweli kwamba rais amechelewa sana kuchukua hatua.

Rais alitangaza uamuzi huo kupitia mkanda uliorekodiwa Jumatatu usiku, akidai kwamba anataka serikali ionekane inapambana kuondoa ufisadi.

LEAVE A REPLY