Waziri Mbarawa auagiza uongozi mpya wa ATCL kufanya mabadiliko ya utendaji

0
228

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameuagiza uongozi mpya wa Shirika la Ndege nchini ATCL kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya miezi mitatu kuanzia leo.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua bodi mpya ya ATCL aliyoiteua baada ya Rais Dk. Magufuli kumteua Mhandisi Ladislaus Matindi kuwa Mkurugenzi mpya wa ATCL na Mhandisi Emmanuel Karosso kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo.

Bodi hiyo ina wajumbe watano kutoka taasisi tofauti ambapo Prof Mbarawa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza malengo ya serikali ya awamu ya tano kwa uweledi na uzalendo.

Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatatua tatizo la wizi wa mali za ATCL hasa mafuta ya kuendeshea ndege na kuhakikisha fedha za shirika hilo zilizopotea zinarudi kuwanufaisha watanzania wote na kuonya kuwa iwapo bodi hiyo haitatekeleza malengo waliyowekewa ataivunja.

Prof. Mbarawa amemuagiza Mkurugenzi wa ATCL kutoa mikataba maalum ya kufanya kazi kwa wafanyakazi wote wa shirika hilo na baada ya miezi sita kuwafanyia tathmini ya utendaji kazi wao na wale ambao watakuwa chini ya viwango watachukuliwa hatua za kiutawala.

Katika kulifufua shirika la ATCL serikali imenunua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 ambapo moja tayari imeshawasili nchini na ya pili inatarajiwa kuwasili nchini kuanzia Jumatatu ya tarehe 27 mwezi huu.

 

LEAVE A REPLY