Waziri Mbarawa aitaka Tazara kupunguza idadi ya mabosi

0
49

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameitaka Menejementi ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kupunguza idadi ya ukubwa wa menejimenti ili kubaki na watu wachache wenye uwezo wa kuzalisha na kufanya kazi kwa weledi.

Amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mfumo maalum wa kieletroniki kwa ajili ya kufuatilia mizigo ya wateja kujua ulipo wakati inasafirishwa na kusaidia kuondoa upotevu.

Alisema licha ya kwamba Tazara imeanza kuboresha miundombinu, kumekuwa na changamoto katika taasisi hiyo ikiwamo suala la uongozi.

Mbarawa alisema ni jambo la kushangaza kuwapo kwa viongozi katika shirika kwa miaka 10 ambao hawana mchango katika uzalishaji, hivyo inabidi menejimenti  kupunguza idara kutoka 15 hadi nane au sita na kuwa na wakurugenzi ambao  watafanya kazi kwa ufanisi.

Aidha, Waziri Mbarawa alizindua mabehewa 10 na vichwa viwili vya treni ambayo alisema yalikuwa mabovu kwa miaka 10 baada ya kupata ajali na sasa Tazara imeyafufua na yanaweza kufanya kazi kwa miaka mingine zaidi ya 15.

Alisema mabehewa hayo ni kwa ajili ya kubebea kokoto na yametengenezwa na wazawa katika karakana ya Tazara iliyoko mkoani Mbeya kwa gharama ya Sh milioni 167 na kwamba yangenunuliwa mapya serikali ingelipia Sh. bilioni 17.

Mbarawa alisema kwa sasa vichwa 10 vya treni ndivyo vinavyofanya kazi kukiwa na mabehewa ya mzigo na ya abiria na kuishawishi Tazara kuona umuhimu wa kununua vichwa vipya angalau kila mwaka kimoja au viwili.

LEAVE A REPLY