Vijana wa CNDD-FDD watuhumiwa kwa ubakaji

0
145
Serikali ya rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi imekumbwa na kashfa mpya baada ya ripoti za kitafiti kudai kuwa umoja wa vijana wa chama tawala unahusika na matendo ya ubakaji kwa wanawake na watoto.
Ripoti hiyo iliyotolewa na taasisi ya Human Rights Watch imesema kuwa matendo ya vijana hao yameongezeka tangu wimbi la maandamano ya kupinga utawala mpya wa Nkurunzinza ulipoanza.
Ripoti hiyo inadai kuwa wengi wa waathirika na wanaolengwa na uhalifu huo ni watu wanaoonekana kuwa na upinzani na uongozi wa rais Nkurunzinza.
Human Rights Watch imedai kuwa ina ushahidi wa msichana wa miaka nane kuvamiwa na kisha kubakwa na kundi la vijana wanne wa Umoja huo mwishoni mwa mwezi wa Aprili mwaka jana.
Ripoti hiyo pia imeendelea kudai kuwa waathirika wengine walifungwa kwa kamba, kupigwa na kubakwa wakiwa wameshikiwa bunduki au visu na makundi ya vijana huku familia zao zikitazama.
Baadhi ya wakimbizi waliokimbilia nchini Tanzania nao wamekaririwa na shirika hilo wakidai kubakwa wakati wa kiondoka Burundi na wengine wakidai kubakwa baada ya kufika kwenye makambi.
Wengi wa waliohojiwa wameelezea kuwa waliowafanyia uhalifu huo ni vijana wa umoja wa vijana wa chama tawala ambao unaogopeka kwa mauaji, upigani na vitisho kwa wafuasi wa vyama vya upinzani.
Pia, maaskari na watu wanaovaa sare za askari wamekuwa wakituhumiwa kwa ubakaji.
Mpaka sasa chama tawala hakijatoa taarifa yake kuhusu tuhuma hizo.

LEAVE A REPLY