Mauaji ya kupigwa risasi mtoto wa miaka 14 kuchunguzwa Angola

0
111

Mamlaka za usalama nchini Angola zimeanza uchunguzi wa mauaji ya mwanafunzi wa miaka 14 yaliyotokea Ijumaa iliyopita.

Mauaji hayo ya kupigwa risasi yalitokea wakati mtoto huyo aliposhiriki kwenye maandamano ya amani yaliyokuwa na lengo la kupinga uvunjwaji wa makazi ili kupisha mradi wa maendeleo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Luanda.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeripoti kuwa askari waliwafyatulia risasi za moto wananchi waliokuwa kwenye maandamano hayo bila ya kuwapa onyo lolote.

Taarifa ya shirika hilo imedai kuwa askari walifyatua risasi za moto hewani pamoja na miguuni mwa wananchi hao ili kuwatawanya lakini risasi mojawapo ikampata shingoni mtoto Rufino Antonio.

Kamanda wa jeshi Lt. Jenerali Simon Carlitos Wala ameliambia shirika la habari la Voice of America kuwa uchunguzi wa tukio hilo unafanyika.

‘Mamlaka zinahitajika kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu sababu za askari kufyatua risasi, kuwafungulia mashtaka waliofanya makosa na kuchukua hatua za kuepuka umwagaji damu wa aina hii kwenye siku za mbele’

Amesisitiza mwakilishi wa HRW Daniel Bekele.

Picha za video zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii na mwanaharakati wa Angola zinamuonyesha mtoto Rufino akiwa amelala chini ya mwembe huku damu zikimwagika kutoka shingoni na watu wakiwa wamemzunguka huku wakiagiza aitwe mama yake.

Mwili wa Rufino uliondolewa maafisa usalama bila kutolewa maelezo yoyote na siku iliyofuatia ulikutwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

LEAVE A REPLY