Tas: Kambi za Albino zifungwe, zinachangia unyanyapaa

0
253

Chama cha watu wenye ualbino (Tas) kimeiomba serikali kuyafunga makambi yote yaliyokuwa yakitumika kuwalinda watu hao dhidi ya mauaji yaliyokuwa yameshamiri katikati ya miaka ya 2000.

Ombi hilo limefuatia uchunguzi wa chama hicho juu ya mtazamo wa watu wengine dhidi ya albino na kugundua kuwa makambi hayo yanachangia watu wasio na ualbino kuwachukulia kwa mtazamo tofauti watu wenye ualbino.

Miongoni mwa dhana zinazodaiwa kuwemo miongoni mwa jamii kuhusu albino ni pamoja na kuonekana kama kundi maalum kwenye jamii ambalo si la binadamu wa kawaida hali inayozidi kuchochea unyanyapaa.

Ofisa uhusiano wa chama hicho, Josephat Tonna ameiomba serikali kulitafakari jambo hilo ili kuiruhusu jamii kuwa na uelewa mpana juu ya tatizo la ualbino kupitia albino wenyewe na wataalamu wa hali hiyo.

Nchini Tanzania kulizuka wimbi la matukio ya ukatili dhidi ya maalbino ikiwemo mauaji na ukataji viungo huku yakihusianishwa na imani za kishirikina hivyo kuilazimu serikali kuandaa kambi maalum kwaajili ya kusaidia ulinzi wa watu wenye ualbino.

Ingawa matukio ya aina hiyo yamepungua kwa asilimia kubwa lakini bado haijafahamika kitafiti iwapo hilo Ia tokeo la uelimishwaji kwa raia au uimarishwaji wa ulinzi pamoja na utekelezwaji wa hukumu za kesi za washtakiwa wa kesi za mauaji dhidi ya watu wenye ualbino.

Picha kwa hisani: Dieter Telemans

LEAVE A REPLY