Tanesco kukata rufaa hukumu ya IPTL

0
134

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme (Tanesco) imepanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICSID) ya Uingereza ya kulitaka shirika hilo kuilipa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) Dola za Marekani milioni 148.4 (Sh bilioni 311).

Fedha hizo ni malimbikizo ya gharama za uwekezaji wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL), Tegeta jijini Dar es Salaam.

Tanesco imesema mpango huo wa kukata rufaa unatokana na kukiukwa kwa sheria na kanuni kadhaa zinazosimamia uendeshaji wa Mahakama hiyo tangu ilipofunguliwa mwaka 2010, ilipotoa uamuzi wa awali mwaka 2014 hadi ilipotoa uamuzi wa mwisho hivi karibuni.

Kutokana na uamuzi huo, Tanesco kwa kumtumia wakili wake Richard Rweyongeza wa Kampuni ya R.K Rweyongeza & Advocate itakata rufaa hiyo ndani ya siku 90 zilizotolewa na Makakama ya ICSID, huku menejimenti yake ikisema ina imani kubwa kwa shirika hilo kupata haki zaidi kuliko ile iliyotolewa hivi karibuni.

Pamoja na uamuzi wa juzi kutokuwa mpya ukilinganisha na ule wa awali uliotolewa na Mahakama hiyo ya Kimataifa Februari 12, 2014, huku ukitoa nafuu zaidi kwa Tanesco, lakini shirika hilo limesisitiza bado yapo maeneo ambayo kama yataangaliwa kwa kina katika rufaa yao yatatoa nafuu zaidi wa uamuzi wa mwisho wa fedha inayopaswa kulipwa, lakini pia mhusika halali wa kulipwa tofauti na ilivyoamriwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba amesema yapo maeneo ambayo Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo imejiridhisha kuwa yalikuwa na udhaifu wa kisheria na hayakutazamwa vizuri na Mahakama ya ICSID katika kufikia uamuzi wa juzi.

Mramba amesema katika uamuzi wa hivi karibuni, Mahakama hiyo ilishindwa kuzingatia uamuzi wake wa awali wa mwaka 2014, na kutoa maamuzi mapya kama vile kesi hiyo imeendeshwa upya, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za uendeshaji wa Mahakama hiyo.

Amesema kanuni za Mahakama hiyo zinasema pande zinazoshtakiana zikifungua kesi ya madai katika mahakama hiyo na tuzo kutolewa, pande hizo haziwezi kufungua kesi upya, na kusema kwa vile Mahakama ya ICSID ilishatoa tuzo katika uamuzi wa awali wa 2014, haikupaswa kubatilisha.

Akitolea mfano alisema katika tuzo ya mwaka 2014, pamoja na mambo mengine, Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kuwa Kiwango cha Marejesho ya Uwekezaji (IRR) ambacho Tanesco wanapaswa kulipa hakitakuwa asilimia 22.31 wala asilimia 0, lakini cha ajabu katika uamuzi wa karibuni Mahakama hiyo ikabatilisha uamuzi wake wa awali na kuagiza Tanesco kulipa kiwango cha asilimia 22.31.

Awali, akielezea ni kwa nini uamuzi wa hivi karibuni ulitoa nafuu kwa Tanesco tofauti na inavyokuzwa na baadhi ya vyombo vya habari (si HabariLeo), pamoja na nia hiyo ya kukata rufaa, Wakili Rweyongeza alisema katika maombi yake, Benki ya Standard Chartered ilitaka ilipwe zaidi ya Dola za Marekani milioni 300, lakini Mahakama hiyo imeamuru kulipwa kwa Dola za Marekani milioni 148.4, hatua ambayo ni ya ushindi kwa Tanesco.

LEAVE A REPLY