SMZ yaipa kipaumbele sekta ya elimu

0
120

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, sekta ya elimu imepewa kipaumbele katika mpango wa maendeleo na kukuza uchumi wa Zanzibar na ipo tayari kukabiliana na changamoto zitakazokwamisha kufikia malengo hayo.

Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein wakati akihutubia wanafunzi wa Shule za Unguja na Pemba katika kilele cha Tamasha la Elimu bila ya malipo hapo katika Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu tangu kutangazwa kwa elimu bure na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, Septemba 23 mwaka 1964, ambapo mafanikio makubwa yamepatikana yakiwemo ya kuwa na vyuo vikuu vitatu nchini.

Dk Shein amesema, katika kipindi cha miaka 20 kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Zanzibar ilikuwa haina vyuo vikuu ambapo wanafunzi wanaohitaji elimu hiyo hulazimika kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam au Makerere au Ulaya.

Amesema, hapo nyuma kabla ya mapinduzi na baada ya mapinduzi, shule ya awali ilikuwa moja ya Saateni, Unguja ikiwa na wanafunzi 60 ya wazazi wenye uwezo kifedha, shule za msingi zilikuwa 62 zikiwa na wanafunzi 22,364,wakati shule za sekondari zilikuwa tano zikiwa na wanafunzi 138.

Rais Shein amesema, mabadiliko makubwa yamefikiwa katika sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 52 baada ya Mapinduzi, shule za awali zipo 286, za msingi ni 365 na sekondari 281.

Amesema katika kufikia azma hiyo, Serikali ya Zanzibar itaendelea na mikakati wa kukuza elimu ya msingi ambayo kwa sasa itatolewa bure na lengo la baadaye ni kuondoa ada katika elimu ya sekondari na azma hiyo itafikiwa uchumi ukiimarika.

Mapema, Rais aliwataka wazazi nao kuwajibika kikamilifu kwa kufuatilia mwenendo wa watoto wao wakati wanapokuwa shule na kazi hiyo wasiwaachie walimu peke yao. Katika hatua nyingine, Rais Shein alitangaza mikakati ya serikali wa kuimarisha sekta ya elimu ambapo shule 10 za ghorofa zitajengwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha, shule 23 zitafanyiwa ukarabati wa kuwezeshwa kupatiwa vifaa mbalimbali vikiwemo vya maabara ya masomo ya sayansi na aliwafariji walimu kwa kuahidi kuyatafutia ufumbuzi madeni sugu yao kwani hilo liko katika ahadi yake.

Akimkaribisha Rais, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema wizara inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu sambamba na walimu kupatiwa mafunzo yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa kazi.

LEAVE A REPLY