Simi aachia ngoma mpya

0
35

Mwanamuziki wa R&B kutoka Nigeria, Simi ameachia kibao chake kipya ‘No Longer Beneficial’ ikiwa ni baada ya kimya cha muda tangu alipoachia wimbo wake uliopita ‘Duduke’.

Katika wimbo huo Simi anaonyesha ufundi wa hali ya juu katika kucheza na sauti huku akiridhisha hisia za mashabiki kwa bembelezo murua katika mahadhi ya Afro – R&B.

Kazi hiyo imefanikishwa na mradi wa utengenezaji vipaji bora vya muziki Afrika Magharibi, Sess na Oscar ambapo Simi ameshirikiana na mumewe ambaye ni mwanamuziki na mbunifu wa Nigeria, Adekunle Gold.

Simi anasema: “Wakati wa mapumziko yangu mafupi kwenye muziki, nilipata wakati mgumu sana. Nilijihisi kama nataka kupasuka kwa ubunifu wa mistari iliyokuwa imejaa kichwani mwangu. Kuna wakati nilihisi kama nipate mtu wa kunihifadhia hiyo mistari.

“Hivyo nilipopata wasaa wa kuandaa ngoma yangu, ikanipa ahueni. Nikapata pumziko na kwa kweli ikanitengenezea kitu cha tofauti upande wa pili.”

Kipaji cha Simi kilianza kuonekana tangu akiwa mdogo, ambapo alikuwa akiimba na kucheza kwenye kwaya ya kanisani kwao, jijini Lagos, Nigeria.

Baadaye alipokuwa mkubwa, aliingia rasmi kwenye muziki mwaka 2014. Baadhi ya nyimbo zake zilizofanya vizuri tangu wakati huo ni pamoja na ‘Tiff’, ‘Jamb Question’ na ‘Love Don’t Care’ alizoimba peke yake.

Nyimbo alizoshirikiana na wasanii wengine ni pamoja na Solder (Falz), No Forget (Adekunle Gold) na ‘So Rire’ (Legendury Beatz).

LEAVE A REPLY