Sethi agoma kuvuliwa uenyekiti wa IPTL

0
367

Mfanyabiashara Herbinder Sethi ameeleza kusikitishwa na hatua ya kumvua uenyekiti wa IPT huku akisema hautambui uongozi mpya uliowekwa madarakani.

Uamuzi wa kumwondoa Sethi katika bodi ya wakurugenzi ambayo pia ilimvua uenyekiti wa IPTL, ulifikiwa baada ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria mikutano ya bodi kwa miezi sita mfululizo bila ruhusa, tangu Juni 19, 2017 alipokamatwa na kushtakiwa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimsomea Sethi mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 22.198 milioni za Marekani (Sh309.5 bilioni).

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa wakili wake, Hajra Mungula iliyotolewa jana kupitia mitandao ya jamii ilisema Sethi hatambui mabadiliko ya uongozi uliowekwa na kwamba yeye ni mmiliki halali wa IPTL ambayo kimsingi inamilikiwa na kampuni anayoimiliki ya Pan African Power Solutions (PAP).

Mungula alisema mabadiliko hayo yamekwenda kinyume na notisi ya katazo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali la Februari 12, 2018 lenye kumbukumbu Na. AGS234 lililozuia aina yoyote ya uhamishaji wa mali na umiliki wa mali za IPTL.

Alisisitiza kwamba licha ya Sethi kuwa na mashtaka ya jinai yanayomkabili, lakini Watanzania wajue bado kampuni hiyo iko chini ya usimamizi salama wa PAP na kwamba madeni yote, madai ya mali na stahiki zote zinazohusiana na kampuni hiyo zipo katika mikono salama.

LEAVE A REPLY