Rais Museveni asema huenda wafungwa wakanyongwa Uganda karibuni

0
118

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema anatafakari uwezekano wa kuanza tena kuwanyonga wahalifu nchini humo.

Museveni amesema hali kwamba yeye ni “Mkristo” imemzuia kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya wale ambao wamehukumiwa kunyongwa.

Hata hivyo, alisema hilo limekuwa likiwatia moyo wahalifu.

“Sijakuwa nikiidhinisha kunyongwa kwa waliohukumiwa kwa sababu mimi ni Mkristo lakini kwa sababu yangu kutokuwa mkali, hilo linawafanya baadhi ya watu kufikiria wanaweza kutenda uhalifu na kuponyoka,” alisema, na kuongeza huenda akaamua kuidhinisha kunyongwa kwa watu kadha.

Ni miaka 13 sasa tangu Uganda ilipotekeleza hukumu ya kifo dhidi ya wahalifu.

Bw Museveni alisema hayo wakati wa sherehe za kuhitumu kwa askari wa idara ya magereza, katika gereza la Luzira mjini Kampala.

Lakini kuna watetezi wa haki za kibinadamu wameshutumu tamko hilo la Rais Museveni na kusema adhabu ya kifo hayikomeshi uhalifu.

Mara ya mwisho Museveni kudihinisha hukumu ya kifo itekelezwe ilikuwa katika gereza la Luzira mwaka 1999.

Kadhalika, aliidhinisha mahakama ya kijeshi kutekeleza hukumu ya kifo mwaka 2005.

Mwaka 1999 watu 27 katika gereza la Luzira hapa mjini Kampala walinyogwa akiwemo Musa Ssebulimbi wa chama cha UPC.

Kwa wakati huu kuna wafungwa 160 wanaosubiri adhabu ya kifo katika gereza la Luzira wakiwemo wanawake sita.

LEAVE A REPLY