Rais Magufuli amuagiza Mwakyembe achunguze mkataba wa TBC na Star Times

0
269

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kuuangalia Mkataba kati ya TBC na Star Times na kuchukua hatua zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa.

Rais hayo amesema hayo jana baada ya kufanya ziara katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amekagua miundombinu ya shirika hilo na kuzungumza na wafanyakazi.

Katika ziara hiyo Magufuli amejionea jinsi miundombinu ya shirika hilo inavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za uchakavu na teknolojia duni na amesema Serikali itafanyia kazi changamoto hizo.

Magufuli hivi karibuni ametoa Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuisaidia TBC amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo, kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.

Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amewahakikishia kuwa Serikali itaboresha stahiki zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo na papohapo amemuagiza Dkt. Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho zote ambazo wafanyakazi hao wanadai kuanzia Mwezi Oktoba 2016, zilizofikia shilingi Bilioni 1 na milioni 285.

Pia Rais Magufuli ametaka wafanyakazi wa TBC kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na ubunifu wa hali ya juu ili matangazo ya chombo hicho cha Taifa yawavutie Watanzania wengi, na kiwe chombo kinachoongoza nchini.

 

 

 

LEAVE A REPLY