Raia wa Korea Kaskazini aomba hifadhi ya kiusalama Hong Kong

0
113

Raia mmoja wa Korea Kaskazini anayedaiwa kuwa mmoja wa wajumbe walioiwakilisha Korea Kaskazini kwenye mashindano ya kitaaluma nchini Hong Kong anadaiwa kuomba hifadhi ya kiusalama kwenye ubalozi wa Korea Kusini huko uliopo Hong Kong.

Ingawa mamlaka zinazohusika zimekataa kutoa undani wa taarifa hiyo lakini gazeti la China  la South China Morning Post limeripoti kuwa mtu huyo alikuwa Hong Kong kwaajili ya kushiriki mashindano ya kitaaluma wiki mbili zilizopita.

Ubalozi huo umeongeza ulinzi na doria ya polisi imeimarishwa kwenye eneo hilo.

Nchi ya China ambayo ina mamlaka juu ya mambo ya kidiplomasia ya Hong Kong imekiri kujulishwa juu ya jambo hilo na kusema kuwa waandishi wa habari hawataruhusiwa kupiga picha kwenye eneo hilo ingawa hakutoa maelezo zaidi juu ya mtu huyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini nayo imekataa kulielezea suala hilo na kutoa msimamo wa serikali ya Korea Kusini kuwa ni kutotolea maelezo yoyote kuhusu watu wanaoiacha Korea Kaskazini na kujiunga na Korea Kusini.

Vyombo vya habari vya ndani ya Hong Kong vinadai kuwa serikali ya Hong Kong inahofia kutokea mgogoro unaofanana na ule wa 2013 unaomhusu Edward Snowden aliyejificha kwenye hoteli ya Hong Kong kabla ya kupanda ndege na kwenda kuomba hifadhi ya muda nchini Urusi.

Chini ya sheria ya msingi ya Hong Kong, China ina mamlaka juu ya mambo ya kidiplomasia na huwarudisha kwao raia wa Korea Kaskazini wanaoingia Hong Kong kinyume cha sheria.

Korea Kusini huwachukua raia wanaotoroka Korea Kaskazini.

Nchi za Korea Kaskazini na Korea Kusini zimekuwa na uhusiano wa mashaka kwa muda mrefu sasa.

LEAVE A REPLY