Polisi wakamata shehena ya mafuta ya kula maeneo ya Tabata

0
103

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekamata shehena ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa kodi wala kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutumika kwa walaji.

Kamanda Sirro amesema Oktoba 10 huko maeneo ya Tabata Ubaya Ubaya, karibu na Chuo cha St Mary’s, askari walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Proches Shayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna mafuta ya magendo yamepitishwa kupitia ufukwe wa Bahari ya Hindi, Mikocheni maeneo ya Mlalakua.

Ameongeza kuwa askari wakishirikiana na maofisa wa TRA walifanya ufuatiliaji mzigo ulipopelekwa ndipo wakagundua mafuta yamepelekwa maeneo ya Tabata na walipofika nyumbani kwa Shayo, walifanya upekuzi na kufanikiwa kukamata mafuta ya kula yenye lebo ya Safi na Oki, madumu 453 ya lita 20 ya thamani ya Sh 14,296,680.

Amesema katika mahojiano, mtuhumiwa ameshindwa kuthibitisha uhalali wa umiliki wa mafuta hayo na kushindwa kutoa nyaraka muhimu. Upelelezi unaendelea na utakapokamilika, mtuhumiwa atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutaifishwa bidhaa husika.

LEAVE A REPLY