Mkuu wa mkoa wa Morogoro ataka uchunguzi fedha za ujenzi mil 500/-

0
271

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, kutuma wakaguzi wa ndani katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro kuchunguza matumizi ya Sh milioni 500 zilizotolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo Tarafa ya Mvuha, wilayani humo.

Dk Kebwe ametoa agizo kwa viongozi wa halmashauri hiyo alipotembelea eneo yanapojengwa makao makuu ya halmashauri ikiwa ni mpango wa kusogeza huduma kwa wananchi.

Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro bado makao yake makuu yapo Morogoro Mjini, hali inayowalazimu wananchi na watumishi wa umma wa kada mbalimbali katika vijiji, kata na tarafa za Ngerengere, Mikese, Mkuyuni, Bwakila, Mvuha na Mkuyuni kusafiri umbali mrefu hadi yalipo ili kupata huduma za kiutendaji na kijamii.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema, ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo ulipata baraka tangu mwaka 1978 wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ukasisitizwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ambapo ilitoa Sh milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi za halmashauri hiyo.

Dk Kebwe amesema kitendo cha ofisi ya makao makuu ya halmashauri hiyo kuendelea kuwepo Morogoro Mjini na kuwafanya wananchi wa vijiji mbalimbali vikiwemo vya Mvuha na Kisaki kulazimika kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 150 kufika mjini hakiwezi kukubalika.

Aliwataka wakuu wa idara za halmashauri hiyo, kuhamia eneo la makao makuu mapya kuanzia Septemba 26, mwaka huu ili kutoa huduma kwa wananchi wakianza kwa kutumia baadhi ya majengo yaliyopo.

LEAVE A REPLY