Mexico: Gazeti lasitisha uchapishaji baada ya mwandishi kuuawa

0
90

Gazeti la Norte de Ciudad Juarez la nchini Mexico limesitisha uchapishaji baada ya mwandishi wa habari kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Katika tahariri yake gazeti hilo limeeleza kuwa chapisho hilo la jana ndilo la mwisho na sababu ya usitishwaji huo ni vifo vya waandishi huku kukikosekana adhabu kwa wanaotenda vitendo hivyo.

Hata hivyo gazeti hilo litaendelea kupatikana kupitia mtandaoni.

Mwandishi wa gazeti hilo, Miroslava Breach, aliyekuwa ripota kutoka mji wa Chihuahua, aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi uliopita.

Breach amekuwa mmoja wa waandishi watatu waliouawa mwezi Machi mwaka huu nchini Mexico.

Mwandishi huyo ametajwa kuandika kwa undani uhusiano uliopo baina ya siasa na uhalifu wa kupangwa kwenye jimbo hilo la Chihuahua kupitia magazeti ya Norte de Ciudad Juarez na gazeti la La Jornada, ambalo husambazwa nchi nzima na lenye makao makuu kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Mexico City.

Breach alipigwa risasi nane akiwa kwenye gari nje ya nyumba yake huku wauaji wakiacha ujumbe usemao ‘Kwa kuwa mdomo mpana’.

Taarifa ya Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari, imedai kuwa tangu mwaka 1992 waandishi wa habari Thelathini na tano wameuawa nchini Mexico kutokana na kazi zao na robo ya hao walipata mateso kwanza na waandishi wengine watatu walifariki kutokana na hatari ya kazi walizopewa.

LEAVE A REPLY