Makamo wa Rais apongeza upandikizaji wa figo

0
196

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kitendo cha Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kufanya upandikizaji figo ni hatua kubwa katika maendeleo ya nchi.

Akizungumza jana mjini hapa, Mama Samia alisema serikali inajivunia hatua hiyo na kwamba inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa aliyepandikizwa figo wiki iliyopita.

Alibainisha kuwa gharama za upandikizaji figo katika hospitali hiyo, ambazo ni Sh. milioni 22 zinaweza kukusanywa katika ngazi za familia na kuokoa maisha ya mgonjwa.

Alipongeza hatua hiyo na kusema itakomboa wananchi wasiokuwa na uwezo, ambao wanaugua ugonjwa huo na kushindwa kwenda India kupata matibabu.

Wiki iliyopita, hospitali hiyo kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Japan ilifanya upasuaji na upandikizaji wa figo kwa mgonjwa mmoja kwa kutumia saa sita.

Upandikizaji huo ulifanywa kwa mgonjwa huyo baada ya mdogo wake wa kike kumpatia figo moja na wagonjwa wote, imeelezwa, wanaendelea vizuri.

Akizungumzia operesheni hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Egid Mubofu alisema upandikizwaji huo umeandika historia na kuleta faraja kwa wakazi wa kanda ya kati, kwa kuanza kutoa huduma hiyo.

Alibainisha kuwa katika watu 100, asilimia 10 ya mkusanyiko huo huugua maradhi ya figo duniani, Akizungumzia gharama za matibabu, Prof. Mubofu alisema nchini India na kwingineko duniani ni kubwa mno.

Alisema hatua hiyo imeweza kuokoa gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi ambapo mgonjwa mmoja nchini India hupandikizwa figo kwa Sh. milioni 77 mpaka 80.

LEAVE A REPLY