Mahakama ya Kenya yamfunga jela kinara wa Ujangili

0
190

Mahakama ya mjini Mombasa nchini Kenya imemkuta na hatia ya ujangili wa kimataifa mtuhumiwa Feisal Mohammed na kumhukumu kifungo cha miaka 20 gerezani.

Feisal aliyepinga kuitwa kiongozi wa kundi la majangili alikamatwa akiwa na pembe za ndovu 413.

Kesi yake ambayo ilifanyika nje ya jengo la mahakama kwenye viwanja vya Kenya Wildlife Service ilichelewa kuanza baada ya mawakili wa mtuhumiwa kupinga eneo ambapo kesi inasikilizwa kwa madai kuwa viwanja hivyo vinamilikiwa na mlalamikaji. Madai hayo yalipingwa na waendesha mashtaka.

Feisal na watuhumiwa wengine watano ambao wameachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kuwatia hatiani walishtakiwa kwa tuhuma za kuwa vinara wa kuua Ndovu (Tembo) na kusafirisha pembe zao nje ya nchi.

Sehemu ya pembe za ndovu anazotuhumiwa kukutwa nazo zikiwa tayari kusafirishwa zilikuwa zimewekwa kwaajili ya kutazamwa na raia karibu na eneo ambalo hukumu yake ilitolewa.

Nchi za Afrika zimekuwa zikikabiliwa na tishio kubwa la kutoweka kwa wanyama hao baada ya ujangili na biashara ya meno ya ndovu kuota mizizi.

LEAVE A REPLY