Mahakama nchini kuanza kuchapa mwenendo wa kesi kieletroniki

0
137

Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na ya Australia Kusini inatarajia kuanzisha utaratibu wa kutumia mfumo wa wapiga chapa maalum watakaochapa maneno ya mwenendo wa kesi mahakamani kwa njia ya kielektroniki.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amesema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Christopher Kourakis.

Othman alisema wamekubaliana na Jaji Kourakis kushirikiana katika kuendesha mashauri kwa njia ya teknolojia, kutoa mafunzo kwa majaji, mahakimu na wasajili wa mahakama pamoja na kuanzisha kada mpya ya wapigachapa maalumu wa mahakama.

Jaji Othman alitoa mfano kuwa nchini Australia Kusini mpiga chapa akiingia mahakamani kesi inaendelea asubuhi ikifika mchana unaweza kupata nakala ya mwenendo, lakini Tanzania inatakiwa uandike kwa mkono kisha upeleke kwa mpigachapa jambo linalochelewesha uendeshwaji wa kesi.

Pia amesema wamemkaribisha Jaji Kourakis kwa ajili ya kuzungumza na kuangalia njia ya kushiriki kwa ukaribu, kwa sababu Tanzania na Australia Kusini ni nchi za Jumuiya ya Madola na kisheria zinatoka kwenye utamaduni mmoja wa Sheria ya Uingereza (Common Law).

Jaji Kourakis alisema yupo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha mifumo ya utoaji haki na kutoa uzoefu wao kuhusu uendeshwaji wa kesi pamoja na utoaji wa adhabu.

Akizungumzia adhabu, Jaji Kourakis amesema wamefuta adhabu ya kifo badala yake, mtu anayepatikana na hatia ya kosa la mauaji, adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 hadi kifungo cha maisha jela, lakini kuna mazingira ambayo jaji anaweza kupunguza adhabu, kama mtu akikiri kosa la mauji, kifungo chake kinaweza kuwa chini ya miaka 20 jela.

LEAVE A REPLY