Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani kuuawa kwa wanajeshi wa Tanzania nchini DRC

0
127
f

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kuuawa kwa wanajeshi 12 wa Tanzania waliokuwa wanalinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Katibu mkuu huyo ameshtumu vikali shambulio hilo na kusema ni sawa na uhalifu wa kivita.Ameitaka DR Congo kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na kusema kwamba waliohusika wanafaa kuwajibishwa.

Wanajeshi zaidi wametumwa eneo hilo na kamanda wa kikosi cha kulinda amani anaelekeza shughuli ya kuwaondoa majeruhi.

Guterres amesema shambulio hilo ndilo mbaya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.

Shambulio hilo lilitekelezwa Alhamisi jioni kwenye kambi ya jeshi ya Semuliki eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema wanajeshi 5 wa jeshi la DR Congo (FARDC) waliuawa pia kwenye shambulio hilo.

Awali, katibu mkuu msaidizi wa Umoja wa Mataifa anayeangazia masuala ya kulinda amani alikuwa ameandika kwenye Twitter kwamba “idadi kubwa” ya wanajeshi walikuwa wameuawa.

Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) chimbuko lao ni Uganda lakini wametuhumiwa kutekeleza mashambulio na visa vya ukatili eneo hilo la DR Congo.

LEAVE A REPLY