Jeshi la Polisi: Abdul Nondo hakutekwa

0
107

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema kuwa Abdul Nondo (24) aliyedaiwa kutekwa wiki iliyopita kumbe hakutekwa bali alisambaza taarifa za uongo na kwamba alikuwa anakwenda Iringa kumtembelea msichana mmoja ambaye jina lake halijawekwa wazi.

 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

 

Amesema kuwa “Huyu mwanafunzi aliyedai kutekwa si kweli, kuna mawasiliano ambayo tumeyakamata alikuwa akifanya na binti mmoja ambaye ndiye alikuwa anamfuata huko Iringa. Alipatikana akiwa mzima wa afya akiendelea na shughuli zake za kawaida, alipelekwa kwa daktari kupimwa na kukutwa hana tatizo lolote la akili.

 

“Baada ya kufanya uchunguzi tumebaini na kujiridhisha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa huru na alifika Iringa akiwa salama. Huo muda anaosema alitekwa saa saba usiku, alikuwa bado anafanya mawasiliano ya meseji ya kawaida na huyo binti aliyekuwa anamtembelea huko Iringa.

 

“Tulitegemea alipoachiwa pengine angeenda kituo cha karibu cha polisi na kujieleza, lakini amekutwa katika mazingira kama nilivyoelezea…. huyu ni mhuni tu kama wahuni wengine. Pengine alilizua hilo ili kutaka kujipatia umaarufu,”.

 

Aidha, Mambosasa amesema baada ya uchunguzi kuendelea walibaini Nondo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akifanya naye mawasiliano ya mara kwa mara wakati akiwa njiani kwenda Iringa, hivyo jeshi hilo linaendelea kumshikilia.

LEAVE A REPLY