Jafo ataka kuundwa kwa Mabaraza ya Walemavu nchini

0
131

Waziri wa TAMISEMI, Suleman Jafo, amewapa mwezi mmoja  makatibu tawala mikoa kuhakikisha wanapeleka taarifa za mabaraza mangapi ya walemavu yaliyoundwa kuanzia ngazi ya kata, wilaya na mkoa yatakayoshughulikia masuala yao hususan elimu.

Jafo alisema  hayo jana wilayani Kisarawe alipokuwa akipokea msaada wa vifaa vya watu wenye ulemavu vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masula ya watu wenye ulemavu la   ADD International.

Alipongeza Wilaya ya Kisarawe kuwa ya kwanza kuunda baraza la watu wenye ulemavu, baada ya waraka huo kutolewa na ofisi yake,  na kusisitiza kuwa mabaraza hayo ni muhimu katika ustawi wa watu wenye ulemavu hasa katika kusimamia elimu.

Katika hatua nyingine, Jafo amemwagiza Kaimu Mkurugenzi  Mtendaji wa Wilaya  Kisarawe, Wanchoke Chinchibera, kuhakikisha wanajenga choo cha mtoto mwenye ulemavu wa miguu wa darasa la tano Shule ya Msingi Kazimzumbwi,  Yusufu Kondo (14), baada ya mtoto huyo kueleza changamoto zinazomkwamisha kielimu, ikiwamo kukosa choo rafiki kutokana na ulemavu.

Pia aliagiza maofisa ustawi wa jamii na maendeleo katika halmashauri zote kuhakikisha wanawatambua watoto wenye ulemavu na kubainisha changamoto zao za msingi na kuzipatia ufumbuzi ikiwamo kuwawezesha  ili kupata elimu kwa kuwa Serikali inatoa kila mwezi  Sh. milioni 23 .8   kwa ajili ya watoto wenye ulemavu kupata elimu katika mazingira rafiki.

Msaada huo wa vifaa vya watu wenye ulemavu umegharimu Sh.  174, 577, 000  na ulitolewa na Mkurugenzi wa ADD International, Rose John, kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu walioko mashuleni katika shule  12  za wilaya za Kisarawe, Mkuranga , Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini.

LEAVE A REPLY