IGP Sirro afanya mabadiliko jeshi la Polisi nchini

0
350

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemteua Naibu Kamishna wa Polisi, Maulid Makabila kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (D/DCI) Zanzibar, huku akifanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.

Kabla ya uteuzi huo, Makabila alikuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia uhalifu makao makuu ya Polisi Dar es Salaam.

Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali anakwenda kuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa polisi, Thobias Sedoyeka aliyekuwa makao makuu ya upelelezi Dar es Salaam.

Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hasina Ramadhani Taufiq anakuwa ofisa mnadhimu makao makuu ya polisi Zanzibar na nafasi yake inachukuliwa na kamishna msaidizi, Haji Abdallah Haji aliyekuwa ofisa mnadhimu Mkoa wa Mjini Magharibi.

Taarifa hiyo inaeleza mabadiliko hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

LEAVE A REPLY