Idriss Sultan afikishwa mahakamani Kisutu

0
303

Mchekeshaji na muigizaji maarufu nchini, Idris Sultan (27) na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shitaka ya kupandisha mahudhui mtandaoni bila leseni kutoka TCRA.

Idriss mwenye umri wa miaka 27 ambaye ni mchekeshaji wa jukwaani amesomewa shitaka hilo akiwa na wenzake katika mahakama hiyo leo Ijumaa.

Wengine walioshtakiwa kwenye kesi hiyo ni Doctor Ulimwengu mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Mbezi na Isihaka Mwinjuma (22) mkazi wa Gongolamboto.

Washitakiwa hao wamesomewa shitaka lao na wakili wa Serikali, Batilda Mushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.

Wakili Mushi amesema kuwa washitakiwa hao wote wanakabiliwa na kesi ya Jinai 60/2020.

Washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8 2016 na Machi 13, 2020 katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa wote watatu wametimiza masharti ya dhamana na wapo nje kwa dhamana na Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 21, 2020 itakaposomwa tena.

LEAVE A REPLY