Balozi afunguka walivyomsafirisha kutoka Urusi Dkt. Shika wa ‘900 itapendeza’

0
207

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Patrick Chokala amefunga jinsi walivyomsafirisha kijasusi Dk Shika (bilionea wa nyumba za Lugumi) kurudi Tanzania.

Balozi Chokala aliyekuwa Urusi kati ya mwaka 2002 na 2008 katika kipindi ambacho sakata la utekwaji wa Dk Shika lilijitokeza, amethibitisha kuwa ni kweli Mtanzania huyo ni daktari na kwamba ni kweli amewahi kutekwa.

Dk Shika anatuhumiwa kuvuruga mnada wa majumba ya mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi uliofanywa na kampuni ya Yono baada ya kufika bei ya kuzinunua nyumba hizo tatu kwa Sh3.2 bilioni, lakini akashindwa kutimiza sharti la kulipa asilimia 25 ya fedha hizo.

Kushindwa huko kulipa kulisababisha awekwe rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa siku sita hadi alipoachiwa kwa kujidhamini mwenywe Novemba 14 na kutakiwa kuripoti kila siku.

Baada ya kutoka polisi kwa dhamana, alieleza mambo mbalimbali ikiwamo kutekwa na kuteswa akiwa Urusi Juni 2004, ikiwa ni pamoja na kukatwa vidole viwili mkono wa kushoto na kimoja mkono wa kulia.

Balozi Chokala ambaye alisema analikumbuka vizuri tukio la kutekwa kwa Dk Shika na jinsi ubalozi ulivyomsaidia asipatwe na kadhia kubwa zaidi.

Amesema kutokana na upekee wa yaliyomsibu Dk Shika, ubalozi ulilazimika kuingilia kati ili kunusuru maisha yake.

Balozi huyo amesema Dk Shika alitekwa na majambazi waliokuwa wanataka fedha ambazo yeye mwenyewe (Dk Shika) alikuwa anajigamba kuwa nazo na kuwashawishi watekaji hao kumfuatilia.

Balozi huyo amesema baada ya kufanikiwa kuwatoroka majambazi hao ambao baadaye walikamatwa na polisi nchini humo kisha kufunguliwa mashtaka, Dk Shika alipelekwa hospitali kwa matibabu akiwa amepoteza vidole kadhaa vya mikono yote miwili.

Alisema majambazi hao walimtesa kwa muda mrefu kwa kuwa mpaka anapatikana vidole hivyo vilikuwa vimeanza kuoza.

Pia Balozi amesema baada ya ubalozi kupewa taarifa zake, ulifuatilia na kugundua kwamba alipelekwa nchini humo na Wizara ya Afya, na alikuwa amelipiwa kila kitu ikiwa ni pamoja na tiketi ya ndege.

LEAVE A REPLY