Babu Tale afikishwa mahakamani na kurudishwa mahabusu

0
154

Meneja wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Babu Tale leo amefikishwa katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kwa kesi ya madai inayomkabili dhidi ya Sheikh Hashim Mbonde.

Kesi hiyo imeahirishwa na Babu Tale kurudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam mpaka hakimu aliyetoa amri ya kukamatwa kwake atakaporejea.

Mahakama hiyo pia leo ilitoa fursa kwa pande mbili zinazohusika katika kesi hiyo kujadiliana lakini baada ya majadiliano hayo pande zote zilirudisha majibu kwa hakimu kwamba hazikufikia maelewano yoyote.

Kipindi cha nyuma mahakama hiyo ilimwamuru Babu Tale alipe Sh. milioni 250 Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde, baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Agustine Shangwa, Februari 18, mwaka juzi, katika kesi ya madai namba 185 ya mwaka 2013, iliyofunguliwa na Sheikh Mbonde aliyewalalamikia ndugu hao kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.

LEAVE A REPLY