Ukweli wa ‘BIFF’ ya Dully Sykes na Mwana FA na Jay Moe

1
1066

Staa wa Bongo Fleva na mmiliki wa Dhahabu Records, Dully Sykes ana kinyongo na rapa Mwana FA, unajua hilo?

Huenda hali hiyo imeshamalizika baina ya mastaa hao wa muziki lakini ukweli kuwa ‘maneno yakishatoka huwa hayarudi kinywani’ na ukweli huo unatokana na kauli za mastaa wa Bongo, Mwana FA ambaye aliwahi kumchana Dully Sykes kwenye moja ya nyimbo zake pamoja na Dully Sykes ambaye ameweka wazi kuwa Mwana FA alikuwa hasimu wake.

Dully Sykes amedai kuwa alikuwa na ugomvi na mastaa wa Hip Hop ndani ya Bongo katika kipindi cha nyuma na ugomvi huo huenda ungebadilisha kabisa mahusiano yaliyopo kwa sasa baina yake na mastaa Mwana FA na Jay Moe.

Dully Sykes amedai kuwa ugomvi mkubwa uliokuwepo baina yake na wasanii wa muziki wa Hip Hop ulisababishwa na hatua yake ya kuanza kubadilisha ladha ya muziki na kuipeleka kwenye kuimba ambayo kwa sasa ni maarufu kama Bongo Fleva.

Mkongwe huyo amedai kuwa baada ya kuanza kuingiza ladha za kuimba kwenye muziki wa Bongo rapa Mwana FA aliandika nyimbo ya INGEKUWA VIPI na kumpiga dongo kwa hatua yake hiyo.

Kwenye nyimbo hiyo Mwana FA anasema: ‘Ingekuwa vipi Dully Sykes angeimba hardcore mashairi kama ya Jay Moe, neno Mwanasesere nna imani lisingekuwepo’.

Dully amedai kuwa kwakuwa yeye ndiye aliyeanzisha matumizi ya maneno ya aina ya Mwanasesere alianza kuandamwa na wasanii wa Hip Hop wakidai kuwa anauharibu muziki wa Bongo Fleva.

Je, msimamo wa Dully Sykes umeleta athari gani kwenye Bongo Fleva?

Kama ulikuwa hujui, Ali Kiba, Diamond Platnumz na wakali wengi wa muziki wa kuimba ni tokeo la muziki wa Mwanasesere wa Dully Sykes. Na kama haitoshi Dully Sykes ni mmoja watu wenye mchango mkubwa sana kwenye muziki wa Diamond Platnumz.

Si kazi rahisi kuleta mapinduzi halisi kwenye tasnia fulani isipokuwa ni hadi pale ambapo utakubali kukataliwa na jamii yako lakini ukaendelea kusimamia uamuzi wako.

1 COMMENT

LEAVE A REPLY